Magonjwa ya Ebola na Marburg
Ebola na Marburg ni maambukizi hatari ya virusi yanayoua ambayo husababisha homa ya damu (hemoraji). Virusi huambukizwa kupitia kugusana moja kwa moja na maji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa. Magonjwa haya yana dalili na njia zinazokaribiana za maambukizi, hivyo kipimo cha maabara kinahitajika ili kutofautisha magonjwa haya mawili.
Milipuko ya Ebola nchini Kongo na Uganda
Kwa sasa kuna mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda.
Hatari ya ugonjwa huo kuenea Ulaya na Norway ni ndogo sana. Ikiwa maambukizi yataripotiwa, mamlaka za afya zimejiandaa vizuri, na kuna hatari ndogo ya kuenea zaidi.
Jinsi ugonjwa wa Ebola na Marburg vinavyoenezwa
Virusi vya Ebola na Marburg vinapatikana katika spishi kadhaa za wanyamapori katika nchi kadhaa za Afrika. Binadamu wanaweza kuambukizwa kutoka kwa wanyama.
Kisha maambukizi yanaweza kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kupitia kugusana moja kwa moja na damu na maji maji mengine ya mwili kutoka kwa mgonjwa. Kwa hiyo, ni wale ambao wako karibu na wagonjwa ndio walio katika hatari ya kuambukizwa. Hasa watu wanaoishi na wagonjwa au wanaowahudumia marehemu ndio walio katika hatari ya kuambukizwa. Aidha, wahudumu wa afya wanaowatibu wagonjwa bila kuchukua hatua za kutosha za kudhibiti maambukizi wako katika hatari ya kuambukizwa.
Unaweza kuambukiza wengine unapokuwa una dalili tu. Hii inamaanisha kuwa huwezi kuambukiza wengine mara tu unapopata maambukizi au ugonjwa unapoanza, hiki ni kipindi ambacho unaambukizwa hadi unapougua. Hatari ya maambukizi huongezeka kadiri ugonjwa unavyoendelea, na huwa kubwa zaidi wakati wa hatua ya kutokwa na damu.
Virusi havienezwi kupitia hewa au kwa ukaribu wa kawaida, kama vile kuwa katika chumba kimoja na mgonjwa au wagonjwa wanaopita barabarani. Pia hakuna hatari yoyote ya kuweza kuambukizwa kupitia mfumo wa kiyoyozi ikiwa uko kwenye ndege moja na mtu ambaye ni mgonjwa. Hata hivyo, huduma ya afya itafuatilia abiria wa ndege ambao walikuwa wamekaa karibu na mgonjwa.
Ugonjwa unapoanza
Muda kuanzia kuambukizwa hadi kupata dalili unaweza kutofautiana kutoka siku 2 hadi 21. Ikiwa hujapata dalili ndani ya siku 21 baada ya kuwa karibu na mgonjwa, basi hujaambukizwa.
Dalili za magonjwa ya Ebola na Marburg
Dalili za awali si maalum na zinaweza kujumuisha
- homa
- baridi
- kutapika
- kuharisha
- maumivu ya kichwa
- maumivu ya misuli na viungo
- uchovu
- maumivu ya tumbo
Baada ya siku 5-7, kutokwa na damu na kushindwa kufanya kazi kwa ogani za ndani ya mwili kunaweza kutokea.
Kiwango cha vifo hutofautiana sana kutokana na mlipuko mmoja hadi mlipuko mwingine (asilimia 20-90), kulingana na upatikanaji wa huduma za afya, upimaji na matibabu.
Homa ya Ebola na Marburg ina dalili zinazofanana, na kipimo cha maabara kinahitajika ili kuthibitisha utambuzi ugonjwa husika. Haiwezekani kupima ili kujua kama umeambukizwa ikiwa bado si mgonjwa.
Matibabu
Hakuna matibabu ya virusi vyenyewe. Matibabu yanajumuisha kutoa huduma bora zaidi na kupunguza dalili.
Njia za kujikinga
Kuna chanjo dhidi ya virusi vya Ebola, lakini kwa sasa zinatumika wakati wa milipuko tu. Kazi inaendelea ili kuzalisha chanjo zaidi, ikiwa ni pamoja na chanjo dhidi ya virusi vya Marburg.
Hatari ya maambukizi kwa watu wanaoishi katika nchi zilizo na milipuko ya Ebola au ugonjwa wa Marburg bila kuwa na ukaribu wa moja kwa moja na wagonjwa ni ndogo sana.
Magonjwa haya yanaweza kuzuiwa kwa
- kuepuka kugusana na wagonjwa au maiti
- kuepuka kugusana kwa karibu na wanyama hai na mizoga, ikiwa ni pamoja na nyani, panya na popo
- kutotembelea mapango na maeneo mengine ambapo popo wanaishi
- kutokula au kuandaa kile kinachoitwa ‘nyama ya porini’, yaani nyama ya wanyamapori
Maswali na majibu kuhusu magonjwa ya Ebola na Marburg
Unapaswa kufanya nini baada ya kurudi kutoka kwenye nchi yenye mlipuko?
Ikiwa haukuwa karibu na mtu aliye na Ebola au Marburg
Ikiwa uko sawa, hauonyeshi dalili za ugonjwa, na haukuwa karibu na mtu yeyote aliye na Ebola au Marburg, haupaswi kuchukua tahadhari yoyote.
Ikiwa utapata homa au dalili zingine baada ya kurudi kutoka kwenye eneo la mlipuko, unapaswa kuwasiliana na daktari, hata kama haukugusana moja kwa moja na mtu yeyote aliye na Ebola au Marburg. Inaweza kuwa muhimu kuangalia magonjwa mengine pia, kama vile malaria. Mwambie daktari kwamba umekuwa katika eneo la mlipuko, ili aweze kuomba taarifa zaidi ikiwa ni lazima.
Ikiwa umekuwa karibu na mtu aliye na Ebola au Marburg
Ikiwa umekuwa katika eneo lenye mlipuko na umekuwa na ukaribu wa moja kwa moja na mtu ambaye ni mgonjwa au amekufa kutokana na Ebola au Marburg, unapaswa kuwasiliana na daktari kwa simu na umwambie kuwa wewe ni mtu wa kufuatiliwa kwa karibu. Hii inatumika ikiwa una dalili au hauna dalili.
Unapaswa kufuatilia mwenyewe dalili kwa siku 21 za kwanza baada ya kuwa karibu na mtu aliyeambukizwa.
Ikiwa una homa zaidi ya nyuzijoto 38° C, unasikia kichefuchefu au hausikii kichefuchefu, unatapika, unaharisha au unatokwa na damu isiyoelezeka:
- Jitenge na wengine ukiwa nyumbani
- Wasiliana na daktari mara moja kwa simu
- Waambie kwamba umekuwa katika eneo lenye mlipuko na kwamba wewe ni mtu wa kufuatiliwa kwa karibu
Ninakwenda kukutana na mtu anayeishi katika nchi yenye mlipuko. Je, ninahitaji kuchukua tahadhari yoyote maalumu?
Ikiwa yuko vizuri na haonyeshi dalili za ugonjwa, hauhitaji kuchukua tahadhari yoyote. Hakuna sababu ya kushauri kutokutana na watu kutoka maeneo yaliyoathiriwa na mlipuko.
Je, kuna mipango gani ya dharura nchini Norway ikiwa kisa cha Ebola au virusi vya Marburg vitagunduliwa hapa?
Ikiwa maambukizi ya Ebola au Marburg yatagunduliwa nchini Norway, mtu huyo atatengwa katika wodi maalumu. Kuna hatari ndogo sana ya ugonjwa kusambaa zaidi ndani ya nchi. Norway iko tayari kukabiliana na hali kama hiyo.
Soma zaidi kuhusu Ebola na Marburg katika Taasisi ya Afya ya Umma ya Norway
- Magonjwa ya Ebola: Kijitabu cha mwongozo kwa wataalamu wa huduma ya afya (taarifa katika lugha ya Kinorwei) (fhi.no)
- Magonjwa ya Marburg: Kijitabu cha mwongozo kwa wataalamu wa huduma ya afya (taarifa katika lugha ya Kinorwei) (fhi.no)
- Ushauri kwa wafanyakazi wa msaada na wataalamu wa huduma ya afya wanaosafiri kwenda maeneo yaliyoathiriwa na milipuko ya virusi vya Ebola au Marburg (taarifa katika lugha ya Kinorwei) (fhi.no)
Maudhui haya yametolewa na kuhakikiwa ubora wake na Folkehelseinstituttet
Ilisasishwa mara ya mwisho 9. Septemba 2026